Tuesday 29 April 2008

Wasomi waukosoa Muungano

na Mwanne Mashugu, ZanzibarSIKU moja baada ya kupita kwa sherehe za miaka 44 ya Muungano, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu visiwani hapa, wamesema mabadiliko kuhusu hadhi ya Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Muungano, ni kasoro kubwa inayopaswa kurekebishwa haraka. Kutokana na kasoro hiyo, wanafunzi hao walishauri Serikali ya Muungano kurejesha haraka utaratibu wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Walisema marekebisho ya sheria yaliyomuondolea hadhi Rais wa Zanzibar kushika wadhifa huo, umeishushia hadhi yake Zanzibar katika nyanya ya kimataifa. Wanafunzi hao walisema hayo walipokuwa katika kongamano kuadhimisha miaka 44 ya Muungano wa Tanzania. Hadhi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano iliondolewa kupitia mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Muungano. “Rais wa Zanzibar mamlaka yake yameondoka katika nyanja za kimataifa na uraia wetu umepotea kwa vile hata misaada inaishia Tanzania Bara,” alisema Khamis Issa Mohammed wa Chuo cha Elimu Chukwani. Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, Haji Habib Kombo alisema kwamba hivi sasa Rais wa Zanzibar analazimika kuingia katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kama waziri asiyekuwa na wizara maalum, jambo ambalo halileti picha nzuri. Aidha, mwanafunzi huyo alibainisha kuwa hata mfumo uliopo, hauonyeshi kinagaubaga mamlaka aliyonayo makamu wa rais. Akifafanua, alisema kuwa licha ya taratibu kueleza vinginevyo, lakini hali halisi inaonyesha kuwa mamlaka ya utendaji ya Waziri Mkuu ni makubwa kuliko ya Makamu wa Rais, suala ambalo linahitaji kuangaliwa upya, ili kurejesha hadhi ya Makamu wa Rais. “Bila ya Zanzibar hakuna Tanzania, na bila ya Afro Shiraz Party hakuna CCM… marekebisho ya katiba yafanyike kumpa hadhi Rais wa Zanzibar,” alisisitiza. Alieleza kuwa mfumo huo mbaya wa Muungano, hauathiri katika masuala ya utawala pekee, bali pia katika nyanja nyingine. Alisema kuwa kutokana na mfumo huo, Zanzibar imekuwa ikiathirika kiuchumi na kutoa mfano kuwa pamoja na elimu ya juu kuwa suala la Muungano, hakuna chuo kikuu hata kimoja kilichojengwa na Serikali ya Muungano visiwani Zanzibar. Kombo alisema kwamba Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kinapaswa kupokea ruzuku kutoka Serikali ya Muungano, badala ya kuendeshwa kwa gharama za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar peke yake kama ilivyo sasa. Issa Kheri wa Chuo cha Elimu Chukwani alisema kwamba kero za Muungano zinachelewa kupatiwa ufumbuzi kutokana na viongozi kutozipa umuhimu. Alisema kwamba zipo ripoti nyingi zilizokusanywa juu ya Muungano, ikiwemo ile ya Tume ya Jaji Robert Kisanga, lakini inashangaza kuwa hadi sasa mapendekezo yake hayajatekelezwa. Alisema kwamba iwapo ripoti ya Jaji Kisanga na Francis Nyalali zingefanyiwa kazi, hivi sasa kero nyingi za Muungano zingekuwa zimeshamalizwa. Alieleza kuwa badala ya kutekeleaa mapendekezo ya Tume ya Jaji Kisanga, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alitumia muda mwingi kumshambulia jaji huyo, kwa kutoa ripoti hiyo ambayo kimsingi ilikuwa inawakilisha maoni ya wananchi. “Tume nyingi zimeundwa ikiwemo ile ya Jaji Kisanga, ikafanya kazi nzuri tu, lakini Rais mstaafu Mkapa akamshambulia kutokana na maoni yaliyopendekezwa na wananchi,” alisema. Alieleza kwamba hakuna njia itakayosaidia kuwa na Muungano bora zaidi ya wananchi kushirikishwa na kuamua kwa kupitia utaratibu wa kura ya maoni. Alisema kwamba hivi sasa historia ya Tanganyika ipo hatarini kupotea, kwa vile baadhi ya Watanzania wanaoishi Zanzibar wanapoambiwa wanatoka Tanganyika, wanahisi kama wanatukanwa. Naye Omar Suleiman, alisema kwamba kero za Muungano haziwezi kutatuliwa kwa makongamano, bali kwa wananchi wa Zanzibar kujenga umoja, ili kuhakikisha matatizo yote ya Muungano yanatatuliwa kwa muda muafaka. Alisema kwamba Zanzibar inashindwa kusonga mbele kutokana na tabia iliyojitokeza ya majungu na kuendeleza tofauti za Unguja na Pemba na hivyo kuzorotesha maendeleo ya wananchi. “Jambo la msingi sisi Wazanzibari tuwe na msimamo, tuache tabia ya fitina na ubaguzi kwa misingi ya Upemba na Uunguja, ili tuweze kusonga mbele kutatua matatizo ya Muungano,” alisema. Alisema Zanzibar hivi sasa ni nchi kamili yenye utawala wake, lakini rais wake hana nguvu nje ya Zanzibar. Akifungua kongamano hilo, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Said Mzee, alisema kwamba Zanzibar inarudi nyuma kutokana na wasomi wake kuwa waoga na kushindwa kujitokeza kudai mambo ya msingi ya nchi yao. Alisema kwamba njia nyingi za kiuchumi Zanzibar zimevurugwa na mfumo mbaya wa Muungano, lakini wasomi wengi wamekaa kimya licha ya wao na jamii kuguswa na masuala hayo. Makamu mwenyekiti huyo alisema vikao vya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi havitasaida kutatua kero za Muungano. Alishauri kuwa watu wengi zaidi washirikishwe katika kujadili masuala ya Muungano, kwa vile mambo hayo yanagusa taifa na si CCM au serikali pekee. Aidha, alisema kuwa udhaifu wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika utekelezaji majukumu yao, umechangia Zanzibar kukabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi yakiwemo yaliyo nje ya Muungano. “Wawakilishi wetu hawana elimu ya kutosha katika kujadili mipango ya maendeleo na kiuchumi, ndiyo maana Baraza la Wawakilishi limedorora, hawa ni wazee wetu tunawaheshimu, lakini ukweli wanaburuzwa na serikali,” alisema. Alieleza kwamba umefika wakati wajumbe wa baraza hilo kufuata nyayo za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe, aliyekubali kujitolea kutetea maslahi ya wananchi na taifa.

No comments: