Monday, 28 April 2008

Wataka rais wa Z`bar awe Makamu wa Rais

Wataka rais wa Z`bar awe Makamu wa Rais2008-04-28 09:03:26 Na Mwinyi Sadallah, ZanzibarWanafunzi wa vyuo vikuu Zanzibar wamependekeza Rais wa visiwa hivyo ashike nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ili awe na hadhi ya kimataifa anapokuwa nje ya nchi. Waliyasema hayo katika kongamano la vijana wa vyuo vikuu Zanzibar lililokwenda pamoja na maadhimisho ya miaka 44 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA). Akizungumza katika kongamano hilo, mmoja wa wanafunzi Bw. Haji Habib Kombo, wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Zanzibar, alisema, marekebisho ya 11 ya Tanzania iliyofuta wadhifa wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais yanapaswa kuangaliwa upya. Alisema mfumo uliokuwa ukitumika miaka ya mwanzo ya Muungano ulikuwa mzuri kwa vile ulimwezesha Rais wa Zanzibar kuwa na hadhi ya kimataifa anapokuwa nje ya nchi kama kiongozi wa Tanzania. Marekebisho ya katiba yaliyofuta Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalifanyika mwaka 1995 na kuweka utaratibu wa kuwa na mgombea mwenza. Alieleza kuwa mfumo wa uongozi katika serikali hivi sasa Waziri Mkuu anaonekana msaidizi wa Rais kuliko Makamu wa Rais. Aidha, alisema kitendo cha Rais wa Zanzibar kuingia katika Baraza la Mawaziri wa Muungano kama Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum hakileti tafsiri inayokubalika katika kuimarisha Muungano. Mwanachuo Yahya Alawi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Mbweni alishauri kero za Muungano zitatuliwe haraka kwani zinachangia kuzorotesha maendeleo ya Zanzibar. Alisema utatuzi ukiendelea kuchelewesha utaleta athari kwa vizazi vijavyo kwa vile wananchi hawatakubali kuendelea na Muungano usio na faida kiuchumi. Alikumbusha kuwa wakati umefika hati ya Muungano kuonyeshwa hadharani ili kama kuna mapungufu yarekebishwe. ``Tuwe na Muungano unaokubalika baina ya pande zote, tunahofia vijana baadaye tutakuja kukamatana kutaka kujua faida na hasara za Muungano,`` alisema mwanafunzi huyo. Issa Kheri kutoka Chuo Kikuu cha Elimu Chukwani alisema ni jambo la kushangaza tume nyingi zimeundwa kushughulikia kero za Muungano, lakini utatuzi haujafanyika. Alisema iwapo mapendekezo ya ripoti ya Jaji Robert Kisanga yangetekelezwa kero nyingi zingekuwa zimetatuliwa. Aliongeza kuwa kuna matatizo mengi ya Muungano na kutaka wananchi kupewa fursa ya kuamua kwa njia ya kura ya maoni kuhusu aina ya Muungano wanaotaka. Akifungua kongamano hilo, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Bw. Said Mzee, alisema uwezo mdogo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi umesababisha visiwa hivyo kuwa na matatizo makubwa. Alisema wawakilishi wanashindwa kukosoa serikali na kutetea kero za wananchi. Bw. Mzee alisema wajumbe wa baraza hilo wanaburuzwa na serikali kutokana kuwa na uwezo mdogo ikilinganishwa na wenzao wa Bunge la Muungano. SOURCE: Nipashe

No comments: