Monday, 9 June 2008

Suluhisho la Zanzibar

na Mwandishi Wetu
WAKATI harakati za kuyafufua mazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar zikionekana kushindwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kina dawa ya kudumu ya mpasuko huo.
Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema mfumo wa majimbo, ambao umeasisiwa na chama hicho, unaweza kuwa suluhu ya matatizo ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar hivi sasa.
Mbowe alisema kuwa kitu kikubwa kinachoumiza vichwa kuhusu masuala ya Zanzibar, ni mfumo unaofaa kwa utawala, kutokana na hali halisi kuonyesha kutoshana nguvu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema CUF imeshaonyesha dhahiri kuwa imekikamata Kisiwa cha Pemba, na kwamba hakuna linaloweza kufanyika hivi sasa kidemokrasia kuzuia nguvu za chama hicho kisiwani humo.
“Kinachotakiwa ni kuwaachia CUF waunde serikali yao huko Pemba na chini ya sera yetu ya majimbo jambo hili linawezekana… tunacholenga katika sera hii ni kuwapa watu uwezo na haki ya kujitawala wenyewe, kuamua aina ya viongozi wanaowataka na kujipangia masuala yao wenyewe bila kuingiliwa na serikali kuu,” alisema.
Mbowe alibainisha kuwa, iwapo hilo litafanyika kwa kuanzisha Jimbo la Pemba, CUF wanaweza kuendesha serikali ya jimbo hilo, kama ambavyo vyama vingine vinaweza kuendesha serikali za majimbo watakakoshinda.
Akifafanua, Mbowe alisema kuwa ingawa wapo baadhi ya watu wanaiona sera hiyo kuwa inaweza kusababisha mgawanyiko, lakini iwapo itafuatwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu, itasaidia zaidi kuwaunganisha Watanzania.
“Mfumo huu utawapa haki na uhuru zaidi watu wa kujipangia mambo yao, hivyo utawafanya wajione huru zaidi,” alisema na kubainisha kuwa katika mazingira kama hayo, manung’uniko yanayoweza kusababisha chuki miongoni mwa wananchi, yatapungua.
Alisema kuwa dhima kuu ya sera hiyo imegawanyika katika sehemu kadhaa, ikiwamo kurekebisha mfumo wa utawala na kuwawezesha wananchi wa eneo husika kuwachagua viongozi wao wenyewe moja kwa moja.
Alisema mfumo wa sasa ambao baadhi ya viongozi wanateuliwa kama vile wakuu wa mikoa na wilaya, unawafanya washindwe kuwatumikia watu ipasavyo, kwani uwajibikaji wao huwa katika mamlaka iliyowateua na si watu wanaowaongoza.
“Ndio maana tuna wakuu wa mikoa ambao wananchi wengi katika mikoa wanayoiongoza hawawafahamu… wanateuliwa kwa utashi wa mtu mmoja tu na hii ni hatari. Tunachotaka sisi kupitia sera hii ni watu kuchagua viongozi wao katika jimbo lao kutokana na jinsi ambavyo wanawafahamu,” alisema.
Pia, alisema sera hiyo inatasaidia kusisimua uchumi, kwani inalenga kuyafanya maeneo tofauti yashindane kiuchumi.
Mbowe, alisema kila jimbo litakuwa na wajibu wa kukusanya mapato yake, na kuyapangia bajeti ya matumizi, huku likiwajibika kutoa mchango wake kwa Serikali Kuu, kutokana na uwezo wake wa kukusanya mapato.
Alisema Serikali Kuu itaachiwa majukumu manne makubwa na aliyataja kuwa ni uhamiaji, masuala ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na masuala ya sarafu na sera za fedha.
“Mtindo wa sasa wa kukusanya mapato yote na kuyaweka kwenye kapu moja (hazina) ni mbaya kwa sababu unawafanya watu wanaodhibiti hiyo hazina wajione kuwa wana fedha, nyingi hivyo kuzitumia hovyo,” alisema.

No comments: