Thursday 22 January 2009

Mambo ya UVCCM Zanzibar

Hivi ndivyo vijana wa CCM walivyoponda raha, Nami nilishuhudia


2009-01-22 10:32:47 Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Kiwango cha fedha ambacho mkutano wa watu 100 wa siku nne wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) zilitafunwa kimegundulika, na sasa kimeacha maswali mengi juu ya matumizi makubwa kiasi hicho wakati umoja huo ukiwa hoi kimapato. Uchunguzi wa Nipashe kutoka vyanzo mbalimbali visiwani Zanzibar ulikofanyika mkutano huo vimesema kwamba kwa wastani matumzi hayo yalikuwa ni nusu bilioni ambazo zilijumuisha usafiri wa ndani, chakula na malazi katika hoteli ya kifahari ya Zamani Kempinski. Fedha hizo ambazo kwa viwango vyovyote ni nyingi kwa hali ya uchumi wa UVCCM ambayo ilisaidiwa fedha za kuendesha mkutano mkuu wa uchaguzi hivi karibuni na mfanyabishara mmoja, hakuna kiongozi yeyote wa umoja huo aliyekuwa tayari kueleza kwamba zilitoka wapi. Kwa wastani, kiasi hicho cha fedha kwa wajumbe 100 kikikokotolewa kila mjumbe atakuwa ametumia walau Shilingi milioni nne katika siku hizo sawa na Shilingi milioni moja kwa siku. Jambo ambalo linazidi kutia shaka na madai kuwa, malipo yote ya mkutano huo mkubwa uliohudhuriwa na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Thabo Mbeki, yaliratibiwa na Januari Makamba ambaye ni msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete anayeshughulikia hotuba na pia ni mtoto wa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba. Hata hivyo, Januari alipotafutwa na Nipashe hakuwa tayari kueleza nafasi yake katika mkutano huo kwani si kiongozi ndani ya UVCCM. Taarifa zilizopatikana juzi zilisema gharama za huduma za malazi ziligawanyika katika makundi manne. Kundi la kwanza la kada ya chini katika chama lilikuwa likilipiwa huduma ya malazi Sh 466,200 kwa siku, kundi la pili lilikuwa likilipiwa Sh 574,200, kundi la tatu lilikuwa likilipiwa Sh 738,00 na kundi la nne lilikuwa likilipiwa Sh milioni 1.9. Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba kiasi cha Sh milioni 200 kati ya fedha zote zilizotumika zimetolewa na mfanyabiashara mmoja (jina tunalo) na nyingine zilizobaki hazijulikani zilikopatikana. Uchunguzi wa Nipashe pia umebaini kwamba pamoja na UVCCM kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha, bado kuna baadhi ya vyumba vililipiwa bila ya wahusika kulala kati ya vyumba 114 walivyokodi kwa sababu wengine walikuwa wanakwenda na kuondoka kutokana na majukumu mengine waliyopangiwa. Imefahamika baadhi ya wajumbe walikuwa pia wakihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) uliofanyika Zanzibar Beach Resort iliyopo Mbweni, kiasi cha kilomita 47 kutoka hoteli ya Kempinski, mkutano wa UVCCM ulipofanyika. Wajumbe wengine walikodiwa katika hoteli ya ya Fairmont iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja na kusababisha huduma za usafiri kwa wajumbe kufikia Sh milioni 6.4. Huduma za malazi zilifikia Sh milioni 216.4 kwa hoteli ya Kempinski peke yake mbali ya gharama nyingine zilizotumika kukodi hoteli ya Fairmont. Aidha, gharama za huduma za chakula kwa wajumbe zaidi ya 100 zilifikia Sh milioni 49.6.Huduma nyingine za kurudufu, uchapishaji na matumizi ya vifaa vya hoteli pia zilitumika. Viongozi wakongwe wa siasa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, (Tanzania Bara), Pius Msekwa, Kingunge Ngombare Mwiru, Mzee Hassan Nassor Moyo, Balozi Job Lusinde, Balozi Juma Mwapachu na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tiafa UVCCM, Hamad Masauni Yussuf, alipopigiwa simu na Nipashe kuzungumzia mkutano huo, alitoa udhuru kwamba asingeweza kuzungumza kwa kuwa alikuwa anahudhuria kikao. Habari kutoka katika kongamano la UVCCM limeeleza kuwa wajumbe wengi waliupongeza uongozi mpya kwa kufanikisha mkutano huo, baadhi ya wajumbe walifurahi kusafirishwa kwa ndege na kuwekwa katika hoteli ya hadhi ya kimataifa. ``Kwa kweli wajumbe wengi wanaupongeza uongozi mpya wa UVCCM kwa kuwahudumia katika hadhi ya kimataifa,`` alisema mjumbe mmoja mwenye cheo cha juu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kusafirishwa kwa ndege kilichukua nafasi kubwa kwa kutolewa shukrani katika kikao hicho. Mkutano huo umezua mjadala mkali baadhi ya wajumbe wakisema hakukuwa na haja ya mkutano huo kufanyika katika hoteli ya bei kubwa wakati CCM inazo kumbi kadhaa za mikutano kwa mfano ukumbi wa CCM Kisiwandui. Aidha, ilielezwa kuwa Hoteli ya Bwawani ambapo chumba ni Sh 50,000 kwa siku ingelitumika kwa mkutano huo na fedha zingebaki kusaidia mambo mengine ya kuimarisha chama. Gazeti hili lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa UVCCM, Isack Francis, alisema hakuna haja ya kuhoji matumizi ya fedha hizo, kwa vile Nipashe haikushiriki kutoa mchango. ``Ninyi mnahoji nini, kwani fedha hizo mlichanga nyie, hili ni suala letu tuachieni wenyewe, hatujawahi kuwaomba hela yoyote, haya matumizi hayawahusu,`` alisema kwa kuhamaki. Francis alisema uamuzi wowote uliohusu kongamano hilo, ikiwemo uteuzi wa hoteli ya kitalii ya Zamani Kempinski ya visiwani Zanzibar, unaihusu UVCCM. ``UVCCM ni taasisi kubwa, ina vyanzo vingi vya fedha, hata hiyo hoteli ya kitalii tuliamua kuitumia kama wanavyoamua watu wengine, hivyo haiwahusu,`` alisema na kukata simu. Kwa upande wake, Januari Makamba, alisema ushiriki wake katika kongamano hilo, ulitokana na mwaliko ambao hata hivyo, hakusema ulitolewa na nani. Makamba aliyesisitiza kutopenda kuzungumza na vyombo vya habari, alisema akiwa katika kongamano hilo, alishiriki kumsaidia Mwenyekiti wa UVCCM, kutekeleza baadhi ya kazi za kongamano hilo. Hata hivyo, alipoulizwa kuzitaja kazi hizo, Makamba, alikataa na kusema suala hilo linapaswa kutolewa ufafanuzi na UVCCM. Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alisema sakata la matumizi ya fedha hizo,linapaswa kutolewa ufafanuzi na UVCCM wenyewe. Alisema Umoja huo ni kama mtoto aliyefikia hatua ya kujitenga katika familia, hivyo kuendesha mambo yake kwa kadri alivyojipangia. ``Hawa UVCCM wanajitegemea kwa vyanzo vya fedha na hata kanuni za matumizi yake...hilo ni swali zuri, watafute wenyewe watoe ufafanuzi,`` alisema.
SOURCE: Nipashe

3 comments:

Kibunango said...

Nyie CHADEMA mambo ya CCM yanawahusu nini? Pesa ni ya CCM na imeliwa na CCM lakini nashangaa inawawawsha CHADEMA

Anonymous said...

Dada yangu,wewe endelea na harakati za kusambaza taarifa na vita dhidi ya hawa mafisadi.

Huyu jamaa anatuambia hizo ni pesa za CCM na si za CUF, kwani wanachana wa CCM ni wa kutoka Kenya?So long as ni fedha za za wananchi, regardless ni wa chama gani, ni budi zikatumika ipasavyo si kuliwa tu na wajanja wachache. It must be born in everyone's mind that when it comes to issues of Public interests hakuna chama hapo. KUwa ni fedha za CCM gives no justification for misuse of such funds.

Ukisema wacha CCM wale fedha vibaya eti ni zao, Kwani mtoto akiwa ni wako basi unaruhusiwa kumfanya unachotaka?

Watanzania ni lazima tuamke sasa na tuseme NO, NO kwa ufidhuli, Ufisadi na Uzandiki ambao tumekuwa tukifanyiwa kwa zaidi ya miaka 40 sasa, Inatoisha, enough is enough now.NO more!Tumechoka.

Nawakilisha.
Mdau toka UK.

Kibunango said...

Na wewe Anonymous aka mdau wa UK..
Pesa ni ya CCM, wewe inakuwashia nini?